What's New
Speeches
Mkereketwa
Official Policy Documents
Official Working Documents


HISTORIA YA UWT TANGU TANU NA ASP HADI KUZALIWA CCM

(Na Dkt. John M.J. Magotti)

Historia ya UWT haiwezi kutenganishwa na historia ya mapambano ya Ukombozi wa Tanganyika na Zanzibar.  Mapambano yaliyoongozwa na Tanganyika African National Union (TANU) na Afro-Shirazi Party (ASP).

Vyama vyote viwili, TANU na ASP, ni matokeo ya kuvunjwa kwa Tanganyika African Association (TAA) na kuunda TANU na kuvunjwa kwa African Association (AA) na Shirazi Association (SA) na kuunda ASP.

Madhumuni ya TANU yalikuwa ni kung’oa ukoloni wa Kiingereza Tanganyika wakati madhumuni ya ASP yalikuwa ni kung’oa Usultani wa Kiarabu na Ukoloni wa Kiingereza Zanzibar.


 

NAFASI YA UMOJA WA WANAWAKE KATIKA MAPAMBANO YA KUDAI UHURU WA TANGANYIKA


Katika mapambano ya Uhuru, Umoja wa Wanawake kama ilivyokuwa kwa Jumuiya za Umoja wa Vijana na Wazazi, ulifanya kazi kubwa ya kueneza na kuimarisha TANU. TANU ilitambua nafasi ya wanawake katika harakati za kudai Uhuru.

 


WANAWAKE KABLA YA TANU

Kabla ya TANU, wanawake waliendelea kukandamizwa na hapakuwepo na usawa baina ya wanawake na wanaume.

 


Wakoloni waliendeleza kwa nguvu mila mbovu za jadi ambazo ziliwaweka nyuma wanawake na matokeo yake wanawake waliendelea kuwa wanyonge.


Ukandamizaji wa wanawake ulijidhihirisha katika mambo yafuatayo:-

(1)         Elimu iliwapendelea zaidi wanaume;

(2)         Wanawake waliokwenda shule walipata kazi za chini;

 

(3)         Ubaguzi katika kazi; kazi za wanaume na kazi za wanawake;

 

(4)         Ujira mdogo kwa wanawake ukilinganisha na ule anaolipwa mwanaume mwenye elimu sawa.

 

WANAWAKE BAADA YA KUZALIWA TANU

 

Mara tu baada ya kuundwa TANU, ilianzishwa Sehemu ya Wanawake katika TANU kwa minajili ya kupambana dhidi ya Ukoloni. Sehemu ya Wanawake ndiyo iliwakusanya wanawake wanyonge wa mijini na vijijini na kuwashirikisha bega kwa bega na wanaume katika harakati za kudai Uhuru. 

 

Mchango wa Wanawake katika Mapambano ya Uhuru:

 

Katiba ya Kwanza ya TANU (1964) ilitambua nafasi ya wanawake, “Kutakuwa na upande wa Wanawake katika Chama, Mwanamke akishaingia katika Chama papo hapo atakuwa amekwisha kuwa mwanachama kuwa upande wa wanawake ….  Kila Tawi la Chama litakuwa na upande wa wanawake na litakuwa katika Chama chini ya Uongozi wa Halmashauri ya Tawi.  Wanachama wanawake na wanaume wote watakuwa sawa”. Sehemu ya Wanawake iliundwa katika TANU 1955 chini ya Uongozi wa Bibi Titi Mohamed.


Majukumu yaliyotekelezwa na Sehemu ya Wanawake yalikuwa:

 

(1)         Kuhamasisha wanawake kujiunga na TANU;

 

(2)         Kueneza TANU mijini na vijijini kwa njia ya kujitolea;

 

(3)         Kulinda Viongozi wa TANU:  Katika hali ya kulinda Chama dhidi ya maadui, wanawake walijipenyeza kwenye vyama vya siasa na vikundi vya upinzani.

 

(4)         Kuimarisha TANU kifedha kupitia shughuli halali mbalimbali ikiwa ni pamoja na dansi.

 

(5)         Kuendeleza wanachama wanawake kijamii na kiuchumi.  Wanawake walianzisha madarasa ya kushona na kufuma, elimu ya watu wazima, biashara ya maduka na migahawa na vikundi vya ushirika.

 

Sehemu ya Wanawake haikuwa na Kanuni wala Katiba yake.  Kanuni na Katiba zilikuwa ni za TANU.  1961 wanawake walifanikiwa kuwa na Kanuni zao ambazo ziliweka mfumo kutoka Tawi hadi Taifa.  Ngazi ya Taifa ilikuwa na Katibu wa Wanawake ambaye alifanya kazi yake chini ya Katibu Mkuu wa TANU.

 

Umoja wa Wanawake wa Tanganyika (UWT) uliundwa na TANU tarehe 02 Novemba, 1962.  Katika mkutano wake wa Uchaguzi wa Viongozi tarehe 07 – 10 Novemba, 1962 wafuatao walichaguliwa:

 

(1)     Bibi Titi Mohamed        -        Mwenyekiti wa UWT;

 

(2)     Bibi Kanasia Mtenga   -        Makamu wa Mwenyekiti;

 

(3)         Rais wa TANU, Mwalimu Nyerere alichaguliwa kuwa Mlezi wa UWT.

 

Kwa nini TANU iliunda UWT?

 

(1)         Ishara ya kutambua mchango waliotoa wanawake katika mapambano ya kudai Uhuru;

 

(2)         Kuwawezesha wanawake kuwa na chombo chao cha kuendeleza ukombozi wao;

 

(3)         Kuondoa vyama mbalimbali vya wanawake na Baraza la Wanawake wa Tanganyika ambalo lilikuwa linapingana na sehemu ya wanawake katika TANU.  Hii ilikuwa ni jitihada ya makusudi ya TANU kujenga Umoja imara wa wanawake wote wa Tanganyika.

 

Uhusiano wa UWT na Vyama vingine vya Wanawake:

 

Uhusiano wa UWT na vyama vingine vya wanawake ulikuwa ni kupitia TANU.  Uhusiano huo ulijidhihirisha kupitia:-

 

  • Mnamo 1962 sehemu ya wanawake katika TANU walikuwa wenyeji wa “All Africa Women Conference” uliofanyika                    Dar es Salaam.

 

Umaarufu wa mkutano huu ulitokana na:-

 

  • Kuunda chombo cha wanawake wote Afrika cha kuendeleza mapambano ya ukombozi wa wanawake;
  • Chombo hiki kilitamka wazi kwamba kitasaidia katika mapambano ya ukombozi katika sehemu zingine za Afrika ambazo zilikuwa bado chini ya Ukoloni;
  • Chombo hiki kilisaidia kujenga mahusiano na vyama vya wanawake wa Afrika.
  • Kujenga urafiki na vyama vya wanawake vya Urusi na China kupitia ziara za mafunzo;
  • Kujenga urafiki wa vyama vya wanawake katika nchi nyingine, kwa mfano, Angola, Siera Leone, Ujerumani Mashariki, Rwanda, Burundi, Zambia n.k.
  • Kujenga uhusiano wa karibu zaidi na Umoja wa Wanawake wa Afro-Shirazi Party.
Ushirikiano baina ya UWT na UW/ASP ulikuwa wa karibu zaidi na hata TANU na ASP zilipangana na kuunda Chama cha Mapinduzi (1977); ilitolewa nafasi kwa wanawake kuwa na Jumuiya yao.

 

NAFASI YA UMOJA WA WANAWAKE WA AFRO-SHIRAZI PARTY KATIKA KUDAI UHURU WA ZANZIBAR

 

Umoja wa Wanawake wa Afro-Shirazi Party (ASP) ulianzishwa rasmi tarehe 04 Julai, 1958 baada ya kuundwa ASP 1957. ASP ilitambua nguvu za wanawake kisiasa. Umoja wa Wanawake wa ASP ulitambua kwamba ASP ndio Chama kitakachowakomboa kwani ndicho chama kilichokuwa kinawasemea na kuwatetea wanyonge.

 

Wanawake wa Zanzibari walibaguliwa katika chaguzi kwa maana kwamba hawakuruhusiwa kupiga kura wala kugombea nafasi katika Baraza la kutunga Sheria.

 

Umoja wa Wanawake wa ASP ulifanya kazi kubwa ya kuwashawishi wanawake na wanaume kuipigia kura ASP wakati wa chaguzi kuu.

 

Umoja wa Wanawake wa ASP walitoa michango yao kwa minajili ya kuimarisha ASP. Katika Uchaguzi Mkuu wa Tatu Juni, 1961 uliotawaliwa na vurugu, baadhi ya wakinamama waliwekwa ndani. Umoja wa Wanawake ASP walitoa michango yao ya fedha kwa kuweka na kulipia Mawakili waliokuwa wakitetea ASP.

 

Wakinamama chini ya Umoja wao walieneza siasa ya ASP Unguja na Pemba kupitia mikutano.

 

Baada ya Mapinduzi ASP iliunda Idara ya Kinamama wa ASP tarehe 19 Machi, 1964.

 

1978 Umoja wa Wanawake wa Tanzania ulizaliwa na kuchukua nafasi ya Umoja wa Wanawake wa Tanganyika na Umoja wa Wanawake wa ASP.

 

HITIMISHO:

 

UWT imetoa mchango kubwa katika maendeleo ya Taifa letu. Hata hivyo yapo mambo ya msingi ambayo yanaonekana kusahauliwa na UWT katika mfumo tuliyomo wa vyama vingi vya siasa. Baadhi ya mambo hayo ni:-

 


Suala la kuhamasisha umma.

 

Kazi ya kuhamasisha umma ni kazi ya kisiasa ambayo inatakiwa kufanywa na vyama vya siasa pamoja na Jumuiya zake . Chama tawala pamoja na Jumuiya zake ndio wenye jukumu la kuonyesha njia katika kuhamasisha umma ili umma uweze kutalekeza Ilani ya Uchaguzi pamoja na mipango mingine ya Serikali. Wakati wa kudai uhuru, Umoja wa Wanawake ulikuwa mstari wa mbele katika kutekeleza jukumu hili la kuhamasisha umma.


Moyo wa kujitolea kufanya kazi za Chama na kazi za Jumuiya.

 

Moyo wa kujitolea unaonekana ulienda na uhuru na mapinduzi. Siku hizi ni nadra kuwaona wanachama na viongozi wakijitolea kufanya kazi za Chama na kazi za Jumuiya.

 


Kuongoza ni kuonyesha njia.

Viongozi katika ngazi zote wanatakiwa kuongoza kwa kuonyesha njia. Viongozi ndio wanatakiwa kuwa katika mstari wa mbele katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi wa Chama chao kwa vitendo siyo kwa maneno matupu. Ilani ya Uchaguzi 2005 inatukumbusha kwamba kizazi cha sasa cha viongozi wa Chama ikiwa ni pamoja na jumuiya zake ni lazima kibadilike katika msimamo na mtazamo. Tukitaka kuleta mabadiliko ya kimsingi ya nchi na jamii yetu kiuchumi na kijamii ni lazima tuachane na tabia ya kulalamikia tu umaskini wa watu wetu. Tunachohitaji sasa ni vitendo.

 

Turejee katika kijitabu alichokiandika Mwalimu Nyerere 1962 Tujisahihishe.

 

Mwalimu aliandika kijitabu hiki baada ya kuona migongano iliyokuwa imeanza kujitokeza kati ya wananchi na viongozi wa Chama na Serikali. Katika kijitabu hiki, Mwalimu alibaini MAKOSA ambayo huzuia UMOJA wowote kuwa IMARA hata ushindwe kutimiza madhumuni yake. Miongoni mwa makosa hayo ni:-

§  Unafsi (ubinafsi):

 

§  Fitina

 

-     Mwalimu anasema kwamba bado tunao wanachama ambao ni wafitini wakubwa bila kujitambua, wafitini hawa ni wabinafsi.

 

§     Woga        

 

-        Tunaogopa kulaumiwa ili tupendwe. Woga huweza kumfanya mtu kuvumilia maovu.

 

§     Kupinga mawazo ya walio wengi

 

-        Wachache wakubali matakwa ya wengi lakini wengi pia wasikilize wachache.

 

§     Unafsi katika kuwachagua viongozi

 

–       kuwachagua viongozi wa njia ya hila, vitisho, rushwa au ujanja ujanja.

 

§     Kosa la kutojielimisha

 

–       kujielimisha ni kutafuta ukweli wa mambo. Mwanzo wa elimu ni kutambua kuwa hatujui kitu. 

§     Kuyafanya mawazo na matakwa ya nafsi zetu kuwa ni mawazo na matakwa ya raia.

 

§     Kuwagawa watu katika makundi, hususan Viongozi waliochaguliwa na viongozi walioajiriwa.

 

WOSIA wa Mwalimu ni kwamba makosa haya yafaa yaondolewe na kuyaepuka katika Chama na Jumuiya zake

 

 

   

Habari Zaidi:

   
     

ccm flag



Email
Links
Contact Us
CCM Creed   Conditions for Membership   Aim and Objectives

Chama Cha Mapinduzi believes that all human beings are equal

 

It is easy to be a member of CCM as its conditions for membership are directed towards an integrity citizen

 

CCM aims at defending the independence of our country and the freedom of its citizens

© COPYRIGHT 2002-2010
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)
P.O. BOX 50, DODOMA - TANZANIA [TELEFAX: +255-22-2185245; EMAIL: katibumkuu@ccmtz.org]